Klabu ya US Monastir imezuiwa na Shirikisho la soka barani Afrika (CAF) kutumia uwanja wao wa Mustapha Ben Jannet baada ya kutokidhi vigezo
US Monastir iko katika Mji wa Sousse ambako Yanga waliweka kambi ya siku mbili kabla ya kuelekea Tunis kuikabili Club Africain
CAF wamewaelekeza US Monastir kufanya marekebisho muhimu katika uwanja wao lakini ni wazi mechi yao ya kwanza ambayo watacheza nyumbani dhidi ya Yanga hawataruhusiwa kuutumia
Yanga sasa itakwenda kuchuana na US Monastir katika dimba la Hammedi Agrebi Olympic, palepale walipopata ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Club Africain na kutinga hatua ya makundi
Kocha Mkuu wa Yanga Nasreddine Nabi amesema mabadiliko hayo ni faraja kwao kwani wangekutana na vurugu nyingi za nje ya uwanja kama wangepelekwa Sousse
Hata hivyo Nabi amesema mchezo dhidi ya Monastir utakuwa mgumu kwani timu hiyo ni bora kuliko Club Africain
"Hizi ni taarifa nzuri kwetu tulikuwa tunapiga hesabu nyingi jinsi ya kucheza Uwanja wa Mustapha Ben Jannet, wanajua tulishinda kule kungekuwa na vurugu kabla ya mchezo"
"Hatua kubwa ni sisi kujiandaa kucheza kwa ubora, watu wasidhani Monastir nkama Club Africain, Monastir wana timu bora zaidi wana mawinga wenye kasi na viungo wa kati bora," Nabi alinukuliwa na gazeti la Mwanaspoti