Baada ya kuanza kuitumikia Yanga, straika mpya wa timu hiyo, Mzambia, Kennedy Musonda, ameweka wazi kuwa anajua miongoni mwa michezo mikubwa hapa nchini ni dabi ya Kariakoo, mchezo kati ya Yanga dhidi ya Simba
Musonda ameweka wazi kuwa ana shauku kubwa ya kucheza mechi hiyo ili awape furaha mashabiki wa Yanga na kujitambulisha zaidi kwenye soka la Tanzania
Musonda ni miongoni mwa wachezaji wanne waliosajiliwa na Yanga kwenye dirisha dogo la usajili, akiungana na Mudathir Yahya, Mamadou Doumbia na Metacha Mnata
Musonda amejiunga na Yanga akitokea klabu ya Power Dynamos vinara wa ligi kuu ya Zambia
Staa huyo alitua nchini siku ya Jumamosi, Jumapili akafanya mazoezi na wenzake Avic Town na siku ya Jumatatu akapewa nafasi kwenye mchezo wa ligi kuu dhidi ya Ihefu, ambapo alitumika kwa dakika 27 wakati Yanga ikiibuka na ushindi wa bao 1-0
"Nashukuru kwa kufanikiwa kupata nafasi ya kucheza mchezo wangu wa kwanza ndani ya Yanga, kocha kwa kuniamini licha ya kwamba nilikosa sehemu kubwa ya maandalizi ya mchezo"
"Nilikuwa na nyakati nyingi nzuri nikiwa Zambia na kupata nafasi ya kucheza michezo mingi hususani ile mikubwa ya dabi, najua hapa Tanzania kuna dabi kubwa ya Yanga na Simba ambayo ni miongoni mwa dabi bora za Afrika, nina shauku kubwa ya kucheza mchezo huo na kuwafurahisha mashabiki," alisema Musonda
Yanga na Simba zitakutana kwenye mchezo wa ligi kuu ambao utapigwa April 09 katika uwanja wa Benjamin Mkapa