Ushindi wa bao 1-0 waliopata Yanga dhidi ya Ihefu Fc jana umewafanya Wananchi waendelee kujichimbia kileleni mwa msimamo wa ligi kwa tofauti ya alama tisa baada ya kufikisha alama 53
Simba inayoshika nafasi ya pili ina alama 44 wakiwa na mechi moja ya kiporo dhidi ya Mbeya City ambayo ilipaswa kupigwa jana
Hata hivyo Bodi ya Ligi iliusogeza mchezo huo mbele hadi leo Januari 18 kwa kuwa Simba wamechelewa kurejea kutoka Dubai walikokuwa wameweka kambi. Sababu ambayo imewashangaza wadau wa soka kwa kuwa kambi hiyo ya Simba ni suala lao binafsi, ratiba waliifahamu na ulikuwa utashi wao kusafiri nje ya nchi wakati ligi ikiendelea
Wengi wanakumbuka Yanga ilivyokataliwa kuahirisha mchezo dhidi ya Kagera Sugar uliopigwa uwanja wa CCM Kirumba Novemba 12. Yanga ilicheza dhidi ya Club Africain Novemba 09 na kusafiri kwa siku mbili kutoka Tunisia na kutua jijini Dar es salaam Novemba 11 mchana
Wakasafiri kwenda Mwanza usiku wa Novemba 11 na Novemba 12 wakacheza na Kagera Sugar mchezo ambao Yanga ilifanikiwa kushinda bao 1-0
Tuachane na sintofahamu hiyo ya ratiba, tangu Yanga ilipopoteza mchezo dhidi ya Ihefu Fc, imeshinda mechi nane mfululizo!
Wananchi wameshinda mechi saba za ligi kuu na mechi moja ya kombe la FA, wakikusanya alama 21 katika mechi hizo saba za ligi
Kimahesabu kama Wananchi wanaweza kushinda mechi nyingine nane (pamoja na mchezo dhidi ya Simba) basi watajihakikishia kutetea ubingwa wao kwa msimu wa pili mfululizo
Katika mechi 10 zilizobaki, mechi saba zinatarajiwa kupigwa uwanja wa Benjamin Mkapa
