Baada ya kupoteza mchezo dhidi ya Ihefu Fc, kikosi cha Yanga kimecheza mechi tano mfululizo pasipo kuruhusu nyavu zao kutikiswa na wapinzani wao
Kipigo cha mabao 2-1 dhidi ya Ihefu Fc kiliwazindua Kocha Mkuu wa Yanga Nasreddine Nabi na benchi la ufundi wakifanya maboresho muhimu katika mfumo wa kujilinda
Yanga ilishinda bao 1-0 dhidi ya Tanzania Prisons, ikaichapa Namungo Fc mabao 2-0, ikaifumua Kurugenzi Fc mabao 8-0 kwenye mchezo wa kombe la FA

Kisha Wananchi wakashinda 3-0 dhidi ya Polisi Tanzania na Coastal Union katika michezo ambao mlinda lango Djigui Diarra aliweka rekodi ya kutodaka mpira wowote kutoka kwa wapinzani
Katika mechi hizo hakukuwa na shuti lililolenga lango kutoka kwa Polisi Tanzania wala Coastal Union

Kwa jinsi Yanga inavyocheza sasa, majukumu ya ulinzi yanaanzia pale mpira unapopotea
Pia kuimarika kwa Khalid Aucho kwenye eneo la kiungo imechangia kwa kiasi kikubwa kwani Aucho anazuia mashambulizi mengi kufikia safu ya ulinzi
Yanga inapopoteza mpira utaona mawinga wanavyorudi haraka eneo la katikati kuungana na viungo wakimuacha Fiston Mayele peke yake mbele
Safu ya ulinzi pia inatekeleza vyema majukumu yake licha ya mabadaliko ya mara kwa mara ambayo Nabi amekuwa akifanya