Klabu ya Yanga leo imefanya hafla ya makabidhiano ya taarifa za kifedha kutoka kwa aliyekuwa Mwenyekiti wa Yanga Dk Mshindo Msolla kwenda kwa Rais Injinia Hersi Said ambaye uongozi wake ulichaguliwa Julai 09 mwaka huu. Hafla hiyo ilifanyika Hotel ya Serena jijini Dar es salaam
Akizungumza katika Mkutano na Wanahabari, Rais wa Yanga Injinia Hersi Said alisema zoezi hilo lilipaswa kufanyika mapema lakini halikufanyika kutokana na kuchelewa kwa ripoti ya mkaguzi wa mahesabu ya klabu ya Yanga
"Najua wengi wanajiuliza kwa nini zoezi hili limefanyika sasa? Ni kwa sababu ya kufuata taratibu, kama mnakumbuka mwezi Julai 2021 Wajumbe wa Mkutano Mkuu waliteua Mkaguzi wa hesabu za klabu kwa msimu wa 2018-19 na 2019-20. Ripoti ya mahesabu ni sehemu ya nyaraka muhimu katika makabidhiano ya uongozi"
"Tunayo furaha kuwaeleza ripoti hiyo imekamilika na Yanga tumepata hati safi na kuwa miongoni mwa Taasisi zenye usimamizi mzuri wa fedha. Tunampongeza Dk Msolla na Kamati yake ya Utendaji kwa kazi nzuri waliyoifanyia klabu hii"
"Leo wanatukabidhi rasmi ripoti hii na tunaahidi kuendeleza kazi nzuri waliyofanya," alisema Injinia Hersi
Dk Msolla amewashukuru viongozi wenzake wa Kamati ya Utendaji ambao uongozi wao uliingia wakati klabu ikiwa katika mazingira magumu
Amesema umoja na ushirikiano ndio silaha pekee iliyowafanya wafanikishe yale waliyoyatekeleza
Dk Msolla ameutaka uongozi wa Injinia Hersi Said kuhakikisha unakamilisha ujenzi wa uwanja wa Kaunda pamoja na usajili wa Wanachama na Mashabiki
Amesema Yanga inaweza kukamilisha miradi yake mikubwa kupitia mashabiki na wanachama wake ambao wako wengi nchi nzima