Kiungo kiraka wa Yanga Farid Mussa amekuwa akitengeneza mabao muhimu ambayo mara nyingi huihakikishia Yanga alama tatu
Ni mara chache sana Farid hufunga mabao hata anapokuwa kwenye nafasi nzuri, mwenyewe anasema anapendelea zaidi kuwatengenezea wengine
"Mimi napendelea kucheza kitimu zaidi na kuwatengenezea wachezaji wenzangu nafasi. Yani hata ikitokea nimebaki na golikipa halafu kuna mwenzangu yuko kwenye nafasi nzuri, nitampa yeye afunge," alisema Farid
Hilo amelidhihirisha katika mechi mbili zilizopita dhidi ya Tanzania Prisons na Polisi Tanzania
Katika mchezo dhidi ya Tanzania Prisons ambao Yanga iliibuka na ushindi wa bao 1-0, Farid alimtengenezea nafasi Feisal Salum 'Fei Toto' kwenye dakika za majeruhi na kufunga bao pekee lililoipa Yanga alama tatu
Katika eneo alilokuwepo, kama angekuwa mchezaji mwingine pengine angejaribu kufunga mwenyewe
Pia akafanya hivyo kwenye mchezo dhidi ya Polisi Tanzania, akimtengenezea nafasi Fiston Mayele kufunga bao la pili katika mchezo huo ambao Yanga ilishinda mabao 3-0
Bao pekee alilofunga katika msimu huu ni kwenye mchezo wa awali ligi ya mabingwa dhidi ya Zalan Fc katika mchezo wa pili ambao Yanga iliibuka na ushindi wa mabao 5-0