Mtendaji Mkuu wa Yanga Andre Mtine amesema baada ya droo ya hatua ya makundi kombe la Shirikisho barani Afrika kufanyika nchini Misri jana, ana imani watafanya vizuri katika michuano hiyo ambayo Yanga inashiriki hatua ya makundi kwa mara ya tatu katika kipindi cha miaka sita
Mtine alisafiri Misri kushuhudia droo hiyo ambapo Yanga ilipangwa kundi D pamoja na timu za TP Mazembe, US Monastir na Real Bamako
Mtine aliyewahi kufanya kazi klabu ya TP Mazembe kwa miaka 12, amesema ile presha waliyokuwa nayo wakati wanasubiri droo hiyo imemalizika na baada ya kuwafahamu wapinzani wao, wanaweza kufanya kitu katika kundi hilo
"Nina Furaha kubwa kwasasa kwa sababu ule wasiwasi nani tunacheza dhidi yake umekwisha. Upinzani ni mkubwa ila kwa ubora wetu sisi Yanga tunaweza kuishinda timu yoyote kwenye kundi letu"
"Kanuni ya mashindano haya ni lazima michezo yako ya nyumbani ushinde na sisi tuna uhakika kwamba tunaweza kufanya hivyo na tunao uwezo wa kuendelea mbele zaidi ya hapa kwenye hatua inayofuata," alisema Mtine
Nae kocha mkuu wa Yanga Nasreddine Nabi amesema timu zote katika kundi D zina nafasi ya kusonga mbele hatua inayofuata hivyo watajipanga kuwa washindani katika kila mechi
"Nafasi iko wazi kwa timu zote, tunakwenda kushindana na timu zenye uzoefu na uwekezaji mzuri lakini nafasi bado iko wazi. Tuna kikosi kizuri na tutakuwa na maandalizi mazuri ya kujiandaa kwenye hatua hii, naamini tutafanya vizuri na tutafuzu," alisema Nabi