Jana Yanga ilicheza mechi ya 47 mfululizo pasipo kupoteza katika ligi kuu ya NBC wakiichapa Singida Big Stars mabao 4-1 na kurejea kileleni mwa msimamo wa ligi
Pamoja na kiwango bora kilichoonyeshwa na vijana wake, Kocha Mkuu wa Yanga Nasreddine Nabi amesema bado timu haijacheza katika ubora anaotaka
Nabi aliwapongeza wachezaji kwa ushindi mnono dhidi ya Singida Big Stars lakini akasisitiza bado kuna makosa wamekuwa wakifanya ambayo wanapaswa kurekebisha
"Tunapaswa kucheza mechi zote kama fainali, tumefunga mabao manne lakini haimaanishi tumecheza vizuri sana. Ziko nyakati tulicheza vizuri lakini ziko nyakati hatukucheza vizuri, yapo maeneo ambayo tunapaswa kujirekebisha" alisema Nabi
Nae Kocha Mkuu wa Singida Big Stars Hans van der Pluijm alisema vijana wake hawakuwa na siku nzuri uwanjani na walizidiwa na wapinzani wao Yanga
Pluijm alisema matokeo hayo yanaakisi tofauti ya ubora wa vikosi kati ya timu yake na Yanga
"Tuliingia tukiwa na lengo la kutafuta alama tatu lakini mambo hayakwenda vile tulivyotarajia. Unapokutana na wachezaji bora halafu ukafanya makosa lazima utaadhibiwa"
"Naweza kusena hatukuwa na siku nzuri, nawapongeza Yanga kwa kupata ushindi"