Rais wa Yanga Injinia Hersi Said amewataka mashabiki na Wanachama kuendelea kuwa na imani na timu yao licha ya kuumizwa na matokeo ya mchezo wa kwanza wa kuwania tiketi ya kufuzu hatua ya makundi kombe la Shirikisho dhidi ya Club Africain
Akizungumza kupitia ukurasa wa Yanga wa Youtube, Hersi alisema uongozi ulitimiza wajibu kwa kuhakikisha timu inapata kila kitu na walikuwa na maandalizi mazuri kuelekea mchezo dhidi ya Club Africain lakini hawakupata matokeo waliyoyahitaji
Hersi amesema hata wao viongozi wameumizwa na matokeo hayo lakini ni lazima wasonge mbele hasa ikizingatiwa wanakabiliwa na mchezo wa marudiano utakaofanyika Tunisia
Hersi amewataka Wanachama wa Yanga kutokubali kuyumbishwa na baadhi ya watu wasioitakia mema Yanga ambao wanatumia baadhi ya kauli zake alizotoa jijini Mwanza kufanya upotoshaji
Amesema Yanga imeyapokea maoni ya wanachama na mashabiki na itafanyika kazi maeneo yaliyoonyesha kuwa na mapungufu
"Tunawapa pole mashabiki wetu na Wanachama kwa matokeo ya jana, pia tumeyapokea maoni yaliyotolewa na mashabiki na Wanachama baada ya mchezo"
"Nataka niwahakikishie nikiwa Rais wa klabu hii, mimi na Kamati yangu ya Utendaji tumeyapokea maoni na tutayafanyia kazi yote yaliyoonekana ni mapungufu na pia yale ambayo yatakwenda kuifanya timu yetu iwe imara zaidi," alisema Hersi