Kama bado hujanunua tiketi yako kuelekea mchezo wa kombe la Shirikisho dhidi ya Club Africain ambao utapigwa Jumatano, basi fanya hivyo sasa ili uwe sehemu ya historia ambayo Yanga imekusudia kuiandika siku hiyo
Wakati huu Yanga imejipanga kwelikweli, makosa yaliyojitokeza katika mchezo dhidi ya Al Hilal, hayatarudiwa, ushindi katika uwanja wa nyumbani ni LAZIMA
Rais wa Yanga Injinia Hersi Said amewahakikishia Wananchi kuwa wamejipanga na watasonga mbele hatua ya makundi ya michuano ya kombe la Shirikisho
Hersi amewataka mashabiki wa Yanga kujitokeza kwa wingi dimba la Mkapa kwani wachezaji wanahitahi hamasa yao
"Nataka niwahakikishie tutasonga mbele kwenda hatua ya makundi, muhimu twendeni tukaishangilie timu yetu, wachezaji wameahidi na wanaonyesha kwa vitendo katika viwanja vya mazoezi," alisema Hersi
Club Africain wamekuwa wazuri sana wanapocheza katika uwanja wao wa nyumbani lakini ni timu inayofungika ikiwa ugenini
Huo ni utamaduni wa timu nyingi za kiarabu, huwekeza zaidi kushinda nyumbani na hucheza kutafuta sare ugenini
Katika hatua iliyopita ya michuano hii, Club Africain walicheza na Kipanga Fc ya visiwani Zanzibar
Mchezo wa kwanza uliopigwa uwanja wa Amaan ulimalizika kwa matokeo ya suluhu ya bila kufungana lakini wakashinda mabao 7-0 kwenye mchezo wa marudiano uliopigwa Tunisia
Hivyo Yanga imejipanga na itahitaji kumaliza mchezo huo hapahapa Dar ili kwenda kucheza kwa tahadhari mchezo wa marudiano kule Tunisia