Wachezaji wa Yanga wameeleza kuwa tayari kwa mchezo wa ligi kuu dhidi ya Simba ambao utapigwa Jumapili, Oktoba 23 katika uwanja wa Benjamin Mkapa
Wakizungumza jana jioni baada ya mazoezi yaliyofanyika Avic Town, kiungo mshambuliaji Feisal Salum 'Fei Toto' alisema wanatambua ugumu wa mchezo huo kwa kuwa unazikutanisha timu majirani na zenye upinzani wa asili
Feisal alisema wachezaji wote wako tayari na wapambana kuhakikisha wanawapa furaha mashabiki wao kwa kuibuka na ushindi
"Tumejiandaa vizuri, tumefuata maelekezo ya mwalimu sasa tuko tayari. Tunajua dabi ni mechi ngumu kwa sababu inakutanisha timu mbili za Kariakoo lakini sisi tunawaahidi mashabiki wetu tutapambana kuhakikisha tunawapa furaha," alisema Feisal
Nao Zawadi Mauya na Kibwana Shomari wamewataka mashabiki wa Yanga wajitokeze kwa wingi katika mchezo huo kwani wanaihitaji sapoti yao katika kuzisaka alama tatu muhimu ili kutimiza malengo yao waliyojiwekea msimu huu
Yanga itakuwa mwenyeji wa mchezo huo ambao utapigwa uwanja wa Benjamin Mkapa kuanzia saa 11 jioni