Kocha Msaidizi wa Yanga Cedric Kaze amesema kwa sasa mkakati wao ni kuona wanafanya vizuri katika michezo mitatu ya ligi kuu inaofuata kabla ya kuelekeza nguvu zao kwenye mchezo wa mtoano kombe la Shirikisho dhidi ya Club Africain ya Tunisia
Yanga iliangukia Kombe la Shirikisho baada ya kutolewa na Al Hilal ya Sudan kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika kwa jumla ya mabao 2-1, hivyo katika droo ya mechi za mtoano kuwania kufuzu hatua ya makundi jana, imepangwa kuanzia nyumbani Novemba 2, mwaka huu dhidi ya Club Africain iliyoitoa Kipanga FC ya Zanzibar kwa jumla ya mabao 7-0.
Kaze amesema wameona ratiba na mpinzani wao watakayecheza naye Kombe la Shirikisho, wataanza kuifuatilia timu hiyo ingawa kwa sasa mawazo yao yameyaelekeza katika mechi za ligi
"Kabla ya kucheza na Club Africain tunakibarua cha michezo mitatu ya ligi ikiwamo Jumapili hii (dhidi ya Simba), kwanza tunahitaji kufanya vizuri katika mechi hizi kabla ya kuwafikiria Club Africain
"Lakini tutaendelea kuwafuatilia ili wakati wa mechi ukifike tuwe tayari na mkakati wa kupata matokeo mazuri," alisema Kaze
Yanga ilirejea mazoezini jana kuanza maandalizi ya mchezo dhidi ya Simba ambao utapigwa Jumapili Oktoba 23 katika uwanja wa Benjamin Mkapa
Kabla ya kuikabili Club Africain Yanga itacheza mechi tatu za ligi dhidi ya Simba, KMC na Geita Gold