Yanga inajivunia rekodi ya aina yake ambayo hakuna timu imewahi kuifikia katika soka la Tanzania
Mechi 42 pasipo kupoteza kwenye ligi kuu, ikicheza zaidi ya siku 500 pasipo kupoteza mchezo katika mashindano yote
Baada ya kulazimishwa sare ya bao 1-1 dhidi ya Al Hilal katika mchezo wa ligi ya mabingwa Jumamosi iliyopita, Yanga inakwenda Sudan wachezaji wakifahamu kazi kubwa iliyo mbele yao
Watahitaji kudhihirisha kuwa mafanikio haya hawakuyapata kwa bahati mbaya bali ni ubora wa kikosi pamoja na mbinu za benchi la ufundi chini ya kocha Mohammed Nasreddine Nabi
Tabia ya timu kubwa ni kutotabirika na inaweza kupata matokeo katika uwanja wowote
Wachezaji wa Yanga wameziona huzuni za mashabiki wao ambao walijitokeza kwa wingi uwanja wa Benjamin Mkapa siku ya Jumamosi kuwapa hamasa
Lakini pia wamezisikia kejeli, dharau na matusi kutoka kwa watani zao, ni wakati wao kwenda kuwafunga midomo na kudhihirisha kuwa wao ni kizazi bora cha wachezaji waliopita Yanga
Kwenye soka hakuna jambo lisilowezekana na wala hakuna kukata tamaa