Kocha Mkuu wa Yanga, Nasreddine Nabi, ameamua kuifungia kazi Al Hilal ya Sudan baada ya kuipigisha timu yake mazoezi mara mbili kwa siku, huku akieleza kuwa anatarajia kufanya kweli ugenini
Awali, Yanga kabla ya kucheza mechi ya kwanza dhidi ya Al Hilal walikuwa wakifanya mazoezi mara moja kwa siku na baada ya kupata matokeo ya sare, Nabi amewafungia kazi wachezaji wake kwa kuwapa program maalum kuelekea mchezo huo wa marudiano utakaopigwa Jumapili wiki hii jijini Khartoum, Sudan.
Kikosi cha Yanga kinatarajia kuondoka Ijumaa kuelekea Khartoum, Sudan kwa ajili ya mchezo huo ambao wanahitaji kupata ushindi wowote ama sare ya kuanzia mabao mawili ili kutinga hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Nabi amesema wamerejea uwanjani kwa ajili ya kufanyia kazi mapungufu yao kwa kuelekea kupambania matokeo chanya katika mechi hiyo ya marudiano.
Amesema wanaendelea na maandalizi kwa kufanya mazoezi mara mbili kwa siku ambapo asubuhi wanafanya saa mbili na nusu na jioni.
"Tumeona madhaifu yetu katika mechi yetu ya hapa nyumbani, sasa tumeyabeba hayo na kufanyia kazi kuhakikisha tunakisuka kikosi imara kumalizia dakika 90 zilizobakia," alisema Nabi