Pamoja na kikosi chake kulazimishwa sare ya bao 1-1 dhidi ya Al Hilal katika mchezo wa ligi ya mabingwa uliopigwa uwanja wa Benjamin Mkapa leo, Kocha Mkuu wa Yanga Nasreddine Nabi amesema bado wana nafasi ya kufanya vizuri katika mchezo wa marudiano utakaopigwa wiki ijayo huko Sudan
Nabi amesema atafanyia kazi mapungufu yaliyojitokeza katika mchezo huo ili kuhakikisha wanafanya vizuri ugenini
"Tumetengeneza nafasi nyingi lakini hatukuzitumia vyema. Unapokosa nafasi nyingi unamuongezea mpinzani kujiamini na ndicho kilichotokea, Al Hilal wakaweza kurejea mchezoni na kusawazisha"
"Walitupa wakati mgumu baada ya kusawazisha kwani wachezaji wetu walihitaji kufunga zaidi na hivyo kusahau majukumu katika ulinzi"
"Tumewaona Al Hilal wanavyocheza hivyo nasi tutajipanga kukabiliana nao huko Sudan. Nawaamini wachezaji wangu, tuna timu nzuri na tutakwenda kutafuta matokeo ya ushindi ugenini," alisema Nabi
Yanga itahitaji kushinda mchezo wa marudiano huko Sudan au kupata sare ya zaidi ya bao moja kuweza kutinga hatua ya makundi
Sare ya bao moja moja itaupeleka mchezo huo kwenye changamoto ya mikwaju ya penati