Maneno yamekuwa mengi kwa nahodha wa Yanga Bakari Nondo Mwamnyeto ambaye wengi wanaona kiwango chake kimeshuka
Katika mechi za hivi karibuni, Kocha Mkuu wa Yanga Nasreddine Nabi amewatumia Dickson Job na Yannick Bangala katika safu ya ulinzi wa kati na hivyo kuibua minon'gono kuwa huenda Mwamnyeto amepoteza nafasi yake kwenye kikosi cha kwanza pia huenda akapoteza kitambaa cha unahodha
Hata hivyo moja ya changamoto inayomkabili Mwamnyeto yawezekana ni uchovu baada ya kucheza mechi mfululizo 'fartigue'
Afisa Habari wa Yanga Ali Kamwe amesema Nabi anatambua Mwamnyeto ni mchezaji aliyecheza mechi mfululizo akiwa na Yanga katika misimu miwili iliyopita
Wakati akiwa Coastal Union, Mwamnyeto pia alikuwa nahodha na alitumika katika kila mchezo hivyo kumfanya acheze takribani misimu minne mfululizo
"Wengi wanaozungumza kuhusu nahodha wetu (Mwamnyeto) kushuka kiwango hawafahamu, ukweli ni kwamba anakabiliwa na uchovu ('fartigue') baada ya kucheza mfululizo. Profesa Nabi ameona ni wakati sahihi wa kumpumzisha baada ya kutumika sana akiwa Yanga, timu ya Taifa na hata wakati yuko Coastal Union, ni mchezaji ambaye kila mechi utamuona uwanjani"
"Mwamyeto atarejea katika ubora wake na wale wanaohoji kuhusu kiwango chake wasubiri, muda si mrefu watamuona uwanjani akiwa bora zaidi," alisema Kamwe