Mshambuliaji kinara wa kuweka mipira nyavuni katika kikosi cha Yanga Fiston Mayele, amesema wanahitaji nguvu ya mashabiki wao kwenye mchezo wa ligi ya mabingwa dhidi ya Al Hilal ambao utapigwa Oktoba 08 katika uwanja wa Benjamin Mkapa
Yanga inahitaji kupata ushindi mnono katika mchezo wa mkondo wa kwanza ili kujiweka katika nafasi nzuri ya kutinga hatua ya makundi ya ligi ya mabingwa baada ya kusubiri kwa miaka 24
Mayele ambaye Al Hilal walijaribu kumsajili katika dirisha la usajili lililopita, amesema Al Hilal hufaidika zaidi na nguvu ya mashabiki wao wanapocheza katika uwanja wa nyumbani hivyo mashabiki wa Yanga nao wanapaswa kuujaza uwanja wa Benjamin Mkapa Oktoba nane kuwapa hamasa wachezaji na kuhakikisha wanaibuka na ushindi mnono
Mayele amesema anaifahamu vizuri Al Hilal kuanzia kwa kikosi, kocha mkuu Frolentine Ibenge aliyewahi kumfundisha AS Vita na mashabiki wake, huku akiwatoa wasiwasi mashabiki wa Yanga juu ya mechi hiyo na kubwa zaidi akiwataka kwenda uwanjani
"Niliifuatilia mechi yao ya mkondo wa kwanza dhidi ya St. George ya Ethiopia lakini pia nawajua baadhi ya watu ndani ya timu ile, wako bora uwanjani pia nje wana mashabiki wenye mzuka wa aina yake, hivyo kama Yanga tukiungana tunaweza kuwashinda"
"Mashabiki kwetu ni mchezaji wa 12, kila Mwanayanga siku hiyo aje uwanjani, watupe sapoti kwa kadri wawezavyo na sisi tutapambana kuhakikisha tunawafurahisha na kutanguliza mguu mmoja mbele kabla ya marudiano," alisema Mayele
Mayele alifunga mabao sita (hat-trik X 2) katika mchezo wa hatua ya awali ligi ya mabingwa dhidi ya Zalan Fc Yanga ikiondoka na ushindi wa jumla wa mabao 9-0
Yuko katika kiwango bora cha kupachika mabao akiweka kambani mabao 12 katika michezo saba ya mashindano msimu huu