Mwezi Oktoba Yanga ina mechi mbili muhimu za ligi ya mabingwa dhidi ya Al Hilal ambazo zitapigwa Oktoba 7-9 na Oktoba 14-16
Ushindi wa jumla utaishuhudia Yanga ikirejea kwenye hatua ya makundi ya michuano ya ligi ya mabingwa barani Afrika wakifanya hivyo kwa mara ya mwisho mwaka 1998 ambapo hatua ya makundi ilihusisha timu nane tu
Ili kuhakikisha wanakuwa na kikosi kamili katika michezo hiyo, wachezaji waliokuwa majeruhi wamewekwa kwenye uangalizi maalum
Barnard Morrison na Djuma Shabani walikosa mchezo dhidi ya Zalan Fc, wanatarajiwa kurejea uwanjani mapema baada ya hali zao kuimarika
Kinara wa mabao Fiston Mayele na Feisal Salum 'Fei Toto' nao walipata majeraha kwenye mchezo uliopita dhidi ya Zalan Fc
Daktari wa Yanga Shecky Mngazija amesema nyota hao wako kwenye uangalizi maalum kama ilivyo kwa Khalid Aucho ambaye amefanyiwa uchunguzi zaidi baada ya kuumia kwenye mchezo wa ligi kuu dhidi ya Mtibwa Sugar
Habari njema kwa Yanga ni kuwa ligi imesimama kupisha mechi za Kimataifa zilizo katika kalenda ya FIFA hivyo nyota majeruhi watakuwa na muda wa kuimarika kabla ya mikiki mikiki ya ligi kurejea na hatimaye mchezo dhidi ya Al Hilal