Denis Nkane ni miongoni mwa vijana wenye vipaji vya hali ya juu katika kucheza mpira wa miguu nchini.
Alianza kufahamika alipokuwa anacheza Biashara akiifungia timu hiyo magoli muhimu katika mechi muhimu.
Nkane kijana mwenye umri mdogo na pia umbo dogo amejipambanua na kuwaonesha wote ambao hawakudhani kuwa kwa umri wake na umbo lake angeweza kufanya mambo makubwa kiasi hiki.
Ameendelea kudhihirisha kuwa yeye ni mchezaji hatari na wa kuogopwa. Denis Nkane alijiunga na klabu ya Yanga wakati wa dirisha dogo msimu uliopita akitokea Biashara na katika mechi yake ya mwisho alifunga goli dhidi ya Namungo mkoani Lindi.
Kujiunga kwake Yanga ilionekana kama anaenda kupotea. Ikumbukwe kuwa Nkane alisajiliwa kwa mahitaji ya kocha mkuu wa Yanga Nasreddine Nabi ambaye amekuwa bingwa wa kuwaendeleza wachezaji kuwa bora zaidi, kuinua viwango vya wachezaji na kusuka timu imara kadiri ya anavyotaka.
Nafasi anazocheza Nkane zina wachezaji walioonekana wamekomaa kiuchezaji kumzidi yeye, kumbe Nabi alikuwa ameona kitu kwa kijana huyu.
Mechi tatu kubwa zilizoonesha kwanini Nabi alimhitaji kijana huyu ni dhidi ya Simba kwenye Ngao ya Jamii,alicheza kwa kiwango cha juu kusaidia timu kupata ushindi huku akiwasumbua mabeki na kukosa magoli kadhaaa.
Mechi ya fainali ya ASFC msimu uliopita ndipo Nabi aliamua kuwaonesha kuwa Nkane ni silaha yake kibindoni baada ya mambo kuwa magumu uwanjani.
Alipoingia kuchukua nafasi ya nahodha Bakari Mwamnyeto watu walipigwa na mshangao na kuona kama Nabi kapagawa kwani timu ilikuwa nyuma kwa magoli 3-2 na hawakutegemea kama yule kijana mdogo kwa umbo na umri angeweza kufanya chochote.
Alipoingia alibadili mchezo na pia ndiye aliyefunga goli la kusawazisha dakika za mwisho na kusababisha mechi iende kwenye matuta na Yanga kuibuka mabingwa wa ASFC.
Mechi ya klabu bingwa Afrika dhidi ya Zalan akiingia kipindi cha pili kuchukua nafasi ya Dickson Ambundo ubao ukisomeka 0-0.
Dakika mbili baadaye alitengeneza goli la kwanza lililofungwa na Fiston Mayele. Aliisaidia timu yake kupata ushindi wa 4-0.
Nkane anatukumbusha mchezaji Mrisho Ngasa wanayefanana kwa maumbo na uchezaji
Hakuna shaka Nkane leo atakuwa na mchango wake kwenye mchezo wa ligi kuu dhidi ya Mtibwa Sugar utakaopigwa uwanja wa Benjamin Mkapa
Nkane alifunga bao pekee la Yanga kwenye mchezo wa mwisho msimu uliopita Yanga ikiibuka na ushindi wa bao 1-0