Kiungo wa Yanga Feisal Salum 'Fei Toto' Jumanne aliwahakikishia Wananchi kupata alama moja muhimu dhidi ya Azam Fc akifunga mabao mawili ya mashuti ya mbali na kuisaidia Yanga kupata sare ya mabao 2-2 katika mchezo wa ligi kuu ya NBC
Feisal amefichua siri yake ya kufunga aina hiyo ya mabao mara kwa mara kuwa ni kufanya mazoezi ya kupiga mashuti
"Siri kubwa ni kuendelea kulifanyia kazi hilo la kupiga mashuti katika uwanja wa mazoezi ndio maana hata kwenye mechi ikitokea huwa nafanya vizuri kutokana ni utamaduni wangu na si kama nabahatisha"
"Hata kocha kwenye mazoezi amenieleza kama nikiendelea kulifanyia kazi hilo na kulitumia katika mechi naweza kufunga mabao aina hii yasiyopungua nane ndani ya msimu mmoja"
"Unajua mabeki wa timu pinzani ikitokea kwangu nimepata nafasi ya kupiga shuti huwa hawaamini kama naweza kufanya hivyo akili zao zinakuwa kwenye mawazo ya mimi kutoa pasi kwahiyo nafanya tukio hilo la kushtukiza na kuipatia timu yangu faida kwa kufunga bao kutokana na shuti la mbali," alisema Feisal
Tangu asajiliwe na Yanga misimu minne iliyopita, mabao mengi ambayo huyafunga Feisal hutokana na michomo yake anayopiga nje ya 18
Achana na ile beauty beauty yake aliyopiga kule uwanja wa CCM Kirumba Mwanza kwenye mchezo wa nusu fainali kombe la FA dhidi ya Simba, mabao mawili aliyowatungua Azam Fc juzi yameendelea kudhihirisha ufalme wake katika kupiga mashuti ya mbali
Feisal ni silaha muhimu kwa Yanga hasa inapokutana na timu ambazo hupendelea 'kupaki basi'