Jana klabu ya Simba ilimtangaza Kocha wa Coastal Union Juma Mgunda kuwa Kaimu Kocha Mkuu wa timu hiyo wakati wakiendelea kusaka kocha mpya
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Simba ni kuwa wamemchukua Mgunda kwa makubaliano maalum yaani kwa lugha nyepesi ni kuwa Coastal Union wamewaazima Simba kocha wao kwa muda!
Nafikiri hili sio jambo lenye afya kwa soka letu, wale wa mijadala ya 'Fair Competition' msimu uliopita wakati GSM walipojitosa kudhamini ligi kuu basi tuwaone wakilizungumza hili
Mpaka wakati huu Juma Mgunda ni kocha wa timu mbili Coastal Union na Simba
Hizi timu zinashiriki ligi moja (NBC Premier League) na zitakutana kwenye michezo ya ligi kuu
Hakuna maelezo ya ufafanuzi ambayo yanaweza kutolewa kuwaelewesha wadau wa soka kuwa Mgunda hawezi kuathiri matokeo ya mchezo pale timu zake zitakapokutana
Ndio! ni timu zake! kwani yeye si ni kocha wa Coastal Union na Simba!
Haya ndio masuala ambayo mamlaka ya usimamizi wa soka nchini ilipaswa kuonyesha ukali wake kwa kuyakataa vikali kwa sababu hayana taswira nzuri na mustakabili wa soka letu
Sidhani kwa wenzetu mambo kama haya hutokea. Kocha anaweza kuazimwa kwa muda kutoka kwenye klabu kwenda timu ya Taifa na sio kutoka klabu moja kwenda klabu nyingine tena zinazoshiriki ligi moja
Ama kwa hakika soka letu kivetu vyetu...!