Wananchi wamelazimishwa sare ya mabao 2-2 dhidi ya Azam Fc katika mchezo wa ligi kuu uliopigwa uwanja wa Benjamin Mkapa
Feisal Salum 'Fei Toto' leo anastahili tuzo ya nyota wa mchezo kwa upande wa Yanga akiwasaidia Wananchi kuondoka na alama moja muhimu
Daniel Amoah aliitanguliza Azam Fc kwenye dakika ya 25 baada ya mpira wake wa kichwa kumpita mlinda lango Djigui Diarra
Yanga ilikwenda mapumziko ikiwa nyuma kwa bao 1-0 ambapo mkufunzi wa Yanga Nasreddine Nabi, alifanya mabadiliko wakati wa mapumziko kwa kuwaingiza Fei Toto na Djuma Shaban katika nafasi ya Dickson Job na Denis Nkane
Mabadiliko hayo yaliisaidia Yanga kurejea mchezoni kwenye kipindi cha pili, Feisal akifunga kupitia shuti la nje ya 18
Changamoto ya krosi bado imeendelea kuitesa Yanga kwani mpira wa kona uliopigwa na Azam Fc kwenye dakika ya 65 uliwasaidia kufunga bao la pili kupitia kwa Ndoye
Hata hivyo Yanga ikapata nafasi ya kurejea mchezoni baada ya kupata mkwaju wa penati, Morrison akiangushwa kwenye eneo la hatari
Haikuwa bahati kwani Djuma Shabani alikosa mkwaju huo
Wakati Wananchi wakipoteza matumaini, Fei Toto akaachia beauty beauty nyingine nje ya 18 na kumshinda mlinda lango wa Azam Fc Ahmada akiisawazishia Yanga bao la pili
Ulikuwa mchezo wenye upinzani mkali na pengine matokeo hayo yanaakisi ugumu wa mpambano huo



