Winga wa Yanga Tuisila Kisinda amebainisha kuwa alisubiri kwa shauku kubwa kukamilika kwa usajili wake na mabingwa hao wa Tanzania
Baada ya kuitumikia Yanga kwa msimu mmoja, akatimkia RS Berkane ambako amecheza msimu mmoja na kufanikiwa kushinda kombe la Shirikisho barani Afrika, hatimaye Kisinda amerejea tena Yanga
Winga huyo mwenye kasi ya kimbunga, amesema Yanga ni kama nyumbani kwani jina lake amelipata hapo kwa Wananchi
"Nimezitumikia Union Maniema na AS Vita za DR Congo, lakini Yanga imenipa jina kubwa zaidi na sio tu kwa kuwafanyia kazi nzuri, ila nikikumbuka siku ya kwanza tu walivyonipokea haraka nilikuwa mchezaji mkubwa"
"Isingekuwa rahisi kukataa kurudi Yanga, ndiyo imenipa jina kubwa hata nikafika Morocco, nilikuwa katika wakati mgumu nikiomba hii hatua ya kurejea Yanga ikamilike. Sasa narudi Yanga, narudi Tanzania nakuja kuendeleza kazi niliyoishia katikati, nakwenda kuungana na familia yangu kushirikiana nao," Kisinda alinukuliwa na gazeti la Mwanaspoti
Kisinda amebainisha kuwa amerejea Yanga ambayo ni tofauti na ile aliyocheza awali, hivyo atakuwa na kazi ya kufanya ili kuhakikisha anapata nafasi ya kucheza
"Yanga hii ni kubwa tofauti na ile ambayo niliiacha, siwezi kucheza kwa kutumia kazi niliyofanya nyuma narudi na akili ya kufanya juhudi kubwa ili nipate nafasi ya kucheza"
"Niliongea na kocha (Nasreddine Nabi) ameniambia anachotaka na nitapambana kwa ajili ya timu, mashabiki wa Yanga wasubiri nakuja kuwafurahisha zaidi"