Winga wa zamani wa Yanga mkongwe Edibily Lunyamila amesema ujio mpya wa Jesus Moloko msimu huu unampa matumaini kuwa atakuwa na mchango mkubwa katika kikosi cha Yanga kwenye mashindano mbalimbali
Msimu uliopita Moloko alianza vyema lakini baadae akapoteza imani ya mashabiki wake ambao wapo waliotamani atafutwe mchezaji mwingine kwenye nafasi yake katika dirisha hili la usajili ambalo litafungwa leo
Lakini baada ya kumshuhudia kwenye mchezo wa Ngao ya Jamii dhidi ya Simba na michezo miwili ya ligi kuu dhidi ya Polisi Tanzania na Coastal Union, hakuna anayetamani kuona Moloko anaondoka Yanga
Lunyamila amesema Moloko amefanyia kazi mapungufu mengi aliyokuwa nayo ingawa bado anahitaji kufanyia kazi kwenye pasi za mwisho na umaliziaji
"Moloko ana kasi, mikimbio ya hatari, ni aina ya winga ambaye mabeki hawatamani kukutana nae kwani muda wote anawafanya wawe na kazi ya kumzuia. Anachotakiwa kufanyia kazi ni umaliziaji wa pasi za mwisho," alisema
Msimu huu Moloko ametoa pasi moja ya bao katika mchezo dhidi ya Coastal Union pia alisababisha penati kwenye mchezo dhidi ya Polisi Tanzania ambapo hata hivyo Fiston Mayele hakufunga