Kiungo mshambuliaji wa Yanga, Stephane Aziz Ki amesema jukumu lake ndani ya Yanga si kufunga tu bali ni maelekezo mengi anapewa na Kocha wake
Ki amesema dhamira ya wachezaji wote katika kikosi cha Yanga ni kushinda pasipo kujali nani anafunga
"Nipo hapa kuipambania timu, ili icheze vizuri na kuwaweka wachezaji wenzangu kwenye nafasi nzuri ya kufanya vizuri, kama ntaweza kufunga nitafunga kwasababu ili uweze kufanya hivyo ni lazima uwe kwenye nafasi nzuri,” alisema na kuongeza;
"Kipaumbele changu cha kwanza ni kuifanya timu ishinde kutokana na mchezo ulivyo na nafurahi kuwa miongoni mwa wachezaji walioisaidia timu kupata matokeo kwenye mechi mbili mfululizo"
Mkufunzi wa Yanga, Nabi amemzungumzia Ki kwamba ni mchezaji anayemtumia sehemu mbili tofauti kama winga ama kiungo mshambuliaji kulingana na mchezo unavyokuwa na wala hana presha nae.
"Nataka awatengenezee wachezaji wengine nafasi za kufunga, ndani ya michezo miwili aliyocheza nimeona uwezo wake wa kuisaidia timu ingawa bado nasisitiza natengeneza kikosi imara," alisema
Nae mshambuliaji kinara wa mabao katika kikosi cha Yanga Fiston Mayele amesema Aziz Ki ni mchezaji wa daraja la juu ambaye ataisaidia sana Yanga msimu huu
"Aziz Ki ni mchezaji wa daraja la juu, anajua sana mpira, akipokea mpira tayari anajua wapi anaupeleka. Huwa ananiuliza anipe pasi za aina gani ili niweze kufunga. Anaweza kukupasia mguuni au kukuwekea kwenye nafasi," alisema Mayele
Katika michezo mitatu aliyocheza, Ki amehusika kwenye mabao mawili ambayo yote alimtengenezea Mayele
Bao la kwanza alitengeneza kwenye mchezo wa Ngao ya jamii dhidi ya Simba na pia kutengeneza bao la kusawazisha katika mchezo wa ligi kuu dhidi ya Polisi Tanzania