Pasipo kupepesa macho wala masikio, yapo matukio mengi ambayo Yanga haijatendewa haki na waamuzi katika michezo mitatu waliyocheza msimu huu mpaka sasa
Hawakutendewa haki kwenye ngao ya Jamii hasa kwa tukio la rafu mbaya aliyofanyiwa Salum Abubakar 'Sure Boy' pia hawakutendewa haki kwenye mchezo wa ligi kuu dhidi ya Polisi Tanzania katika matukio mengi tu
Jana kwenye mchezo dhidi ya Coastal Union pia hawakutendewa haki kwa tukio la nahodha wa Coastal Union Mtenje Albano kumfanyia rafu mbaya Yannick Bangala
Mtenje huyohuyo baadae akamfanyia madhambi Feisal pasipo kuchukuliwa hatua yoyote
Kocha Mkuu wa Yanga Nasreddine Nabi jana alieleza masikitiko yake vile vijana wake wanavyohatarishiwa maisha yao pasipo kulindwa na waamuzi
Nabi alisema jukumu la waamuzi sio kuwalinda wachezaji wa Yanga tu, bali hata kwa timu nyingine zote kulingana na sheria 17 za soka
Wanayanga msichoke kulalamika pengine mamlaka za usimamizi wa soka zitasikia kabla hayajatokea maafa viwanjani
Swali la kujiuliza ni kwa nini hawa waamuzi wanashikwa na kigugumizi kuchukua hatua kwa mujibu wa sheria hasa kwenye mechi za Yanga?
Kinachoendelea sasa kinatoa uhalali wa kuamini yale maneno ya mitaani kuwa pengine wanapewa maagizo
Kwa sababu haiwezekani matukio mengine yako wazi sana, lakini ni ngumu sana kwa wamuzi kuchukua hatua
Lakini tukio hilohilo likifanywa na mchezaji wa Yanga, hatua huchukuliwa haraka sana
Nafikiri bodi ya ligi inapaswa kuchukua hatua kukomesha haya yanayoendelea, waamuzi wanapaswa kutimiza wajibu wao kwa kuzingatia sheria za mpira wa miguu