Kocha Mkuu wa Yanga Nasreddine Nabi amesema kikosi chake kiko tayari kwa ajili ya mchezo wa Ngao ya Jamii dhidi ya Simba ambao utapigwa kesho Jumamosi katika uwanja wa Benjamin Mkapa
Akizungumza katika Mkutano maalum na Wanahabari kuelekea mchezo huo, Nabi amesema anafahamu ukubwa wa mchezo huo hivyo wamefanya maandalizi mazuri yanayowapa matumaini ya kuibuka na ushindi
"Ninajua umuhimu wa mchezo huu, tumejiandaa vyema. Morali ya wachezaji iko juu, nimependa utayari wao na inanipa matumaini ya kupata matokeo mazuri Tutajitolea kwa uwezo wetu wote tushinde," alisema Nabi
Nabi amebainisha kuwa wachezaji wako tayari kwa mchezo huo isipokuwa mshambuliaji Lazarus Kambole ambaye alipata majeraha kwenye mchezo wa kirafiki dhidi ya Namungo Fc
Nabi amesema winga Jesus Moloko atakuwa sehemu ya kikosi siku ya kesho baada ya kupona majeraha ambayo nae aliyapata katika mchezo wa kirafiki dhidi ya Namungo Fc
"Moloko (Jesus) na Kambole (Lazarus) waliumia kwenye mchezo wa kirafiki dhidi ya Namungo, Moloko yuko tayari kurejea kikosini lakini Kambole bado. Pia tuna wachezaji wageni ambao wako tayari na tunaweza kuwatumia siku ya kesho ingawa wapo wengine tutaendelea kuwaingiza kikosini taratibu"
Nahodha wa Yanga Bakari Nondo Mwamnyeto amewataka mashabiki wa timu hiyo kujitokeza kwa wingi dimba la Mkapa kuwapa sapoti wakiwa na dhamira ya kutetea Ngao ya Jamii waliyoshinda msimu uliopita