Aliyekuwa Mtendaji Mkuu wa Yanga Senzo Mazingisa amesema ataendelea kuwa shabiki na Mwanachama wa Yanga
Mkataba wa Senzo umemalizika Julai 31 Yanga ikimtangaza Wakili Simon Patrick kuwa Mtendaji Mkuu katika kipindi cha mpito
Senzo aliomba kutohuisha mkataba wake kukiwa na taarifa kuwa anataka kurejea Afrika Kusini awe karibu na familia yake
"Ni uamuzi wangu kwa mustakabali wa maisha yangu, hakuna kibaya chochote kinachoniondoa hapa Yanga, hii ni familia yangu nami ni mwananchi hili naomba watu walielewe rasmi kutoka kwangu," alisema Senzo
"Nimeona watu wananiuliza kama narejea Simba au nakwenda Azam niwambie hapana sitakwenda huko nakwenda kufanya kazi zangu nje ya Tanzania, mimi ni mwanachama wa Yanga na nina kadi ya uanachama na nimefurahi sana kufanya kazi hapa nchini"
Senzo amesema ana imani kubwa na uongozi wa Rais Mpya wa Yanga, Injinia Hersi Said na kwamba uongozi huo utafanya makubwa ndani ya klabu hiyo na yuko tayari kuwashauri wakati wowote.
"Hersi ni rafiki na kaka yangu pamoja na Arafat (Haji) na wajumbe wote wa Kamati ya Utendaji, bahati mbaya naondoka wakati sijafanya nao kazi lakini wote nimekuwa nikishikiana nao vizuri ndani na nje ya klabu"
"Naamini mambo yatakuwa mazuri zaidi katika utawala huu,wananchi wenzangu wawape viongozi ushirikiano, nawashukuru serikali ya Tanzania, mamlaka ya vibali vya kazi, shirikisho la soka, Bodi ya Ligi na wote niliyoshirikiana nao hapa, naamini kila mmoja alifurahia jinsi tulivyoshirikiana"