Msimu uliopita Yanga ilikwenda Morocco kuweka kambi ya maandalizi ya msimu mpya. Hata hivyo kambi hiyo ilidumu kwa takribani siku tano tu baada ya kuibuka changamoto za hapa na pale
Changamoto ya covid-19 na wachezaji wengine kuitwa timu za Taifa, ilipelekea Yanga kusitisha kambi August 24 kurejea Tanzania huku wachezaji wengine wakibaki Morocco kusubiri majibu ya covid-19
Nusu ya wachezaji walirejea Dar August 28, siku moja kabla ya kilele cha wiki ya Mwananchi
Matokeo yake Yanga ikapoteza mchezo wa wiki ya Mwananchi dhidi ya Zanaco na baadae kupoteza mechi mbili za ligi ya mabingwa dhidi ya Rivers United baada ya kukosa maandalizi mazuri
Viongozi wa Yanga msimu huu wamejifunza, pengine ndio sababu wamefuta kambi ya Uturuki baada ya muda kutokuwa rafiki
Baada ya msimu mrefu uliokuwa na mafanikio kwa Yanga, ilikuwa ni lazima kwa wachezaji wapate muda wa kupumzika
Yanga ilimaliza mashindano yote Julai 02 kwa mchezo wa fainali kombe la FA dhidi ya Coastal Union
Kiuhalisia kwa muda uliobaki kuelekea wiki ya Mwananchi (August 06), haitakuwa na faida Yanga kwenda kuweka kambi nje ya nchi
Watapoteza muda mwingi safarini kwenda na kurudi wakati wakiweka kambi hapa nchini watahitaji saa chache tu
Hapa Tanzania yapo maeneo tulivu ambayo Yanga inaweza kuweka kambi kujiandaa na msimu mpya kama Black Rhino Academy (Karatu) na hata Morogoro (Bigwa)
Kiuhalisia wanaweza kuamua kubaki hata palepale Avic Town kufanya maandalizi yao, huu utaratibu wa kwenda kuweka kambi nje ya nchi ni katika 'kunogesha' tu
Msimu uliopita Yanga ilikosa maandalizi mazuri tofauti na watani zao Simba ambao walikwenda Morocco mapema na kukaa huko kwa takribani wiki tatu
Lakini kwenye Ngao ya Jamii wakapasuliwa na Yanga ambayo kambi yao ilikumbwa na majanga
Iwe Uturuki, Karatu, Morogoro au hata Avic Town mazoezi watakayofanya wachezaji ni yaleyale