Kocha Mkuu wa Yanga Nasreddine Nabi amewapongeza viongozi chini ya Rais Injinia Hersi Said kwa kufanikiwa kukamilisha usajili wa kiungo mkabaji Gael Bigirimana raia wa Burundi
Bigirimana aliyewahi kuitumikia klabu ya Newcastle United ya Uingereza, alitambulishwa Jumamosi Julai 09 baada ya uchaguzi Mkuu wa Yanga ambao ulimuweka madarakani Hersi kuwa Rais wa klabu
Nabi amesema pamoja na kikosi chake kuwa na viungo bora, Bigirimana analeta kitu tofauti ambacho alikikosa katika viungo wote aliokuwa nao
"Wakati tumepata taarifa tunaweza kumpata Bigirimana nilimuomba Mungu tufanikiwe, hatukuwa na kiungo wa aina yake anayejua kutengeneza muunganiko wa eneo la kiungo la kati," Nabi amenukuliwa na gazeti la Mwanaspoti
"Naona watu wanazungumzia juu ya kwanini hajafunga huko Ulaya, sioni kama ni akili sawasawa ya kujadili kuhusu mtu bora kama huyu,najua jinsi ya kumtumia Bigirimana hapa ili Yanga iwe timu ya hatari zaidi"
"Tuna Sure boy, Aucho, Feisal na Mauya lakini ubora mkubwa wa hawa watu wanne tunaongeza na nguvu ya Bigirimana, ni mchezaji mzoefu anayejua kutengeneza ugumu mkubwa wa eneo letu la kiungo"
Nabi pia amepongeza usajili wa kiungo mshambuliaji Stepnane Aziz Ki akibainisha kuwa anafahamu tayari mchezaji huyo amesajiliwa na Yanga na atawaongeza ubunifu katika safu ya ushambuliaji
"Hii ni zawadi kubwa kwa mashabiki wa hii klabu, ni kazi bora ambayo Hersi aliifanya nimefurahi uamuzi wa wanachama kumchagua, ni kijana anayepigana kwa ajili ya hii klabu sio rahisi kumpata mchezaji kama huyu kuja kucheza Tanzania"