Mtendaji Mkuu wa Yanga Senzo Mazingisa amesema hana shaka na ujio wa winga Bernard Morrison huku akiwataka mashabiki wasahau yaliyopita na wampokee kwa mikono miwili
Senzo amesema kwake ni faraja kuona Morrison amesajiliwa na Yanga kwani ni mchezaji aliyekuwa akimuhofia zaidi katika klabu ya Simba
"Nilifanyia kazi kwa kiasi uhamisho wa Morrison aliposajiliwa na Simba lakini wakati nikiwa Simba nilikuwa namuogopa sana alikuwa hatari sana siku ambayo aliifunga Simba niliumia sana na nikawaambia huyu jamaa watani wetu wamepata mtu hatari,"alisema Senzo
"Nafurahi alipokwenda Simba hakufanikiwa kutufunga ningeumia zaidi ingekuwa kama ametonesha kidonda changu na sasa nilihakikisha anarudi hapa Yanga"
"Mashabiki nawaomba mimi Senzo wasahau wampokee Morrison, watafurahia kazi yake huyu ni mchezaji hatari"
Morrison ametua Yanga akiwa mchezaji huru baada ya kumaliza mkataba na klabu ya Simba
Ni miongoni mwa wachezaji watatu wapya ambao Yanga imewatambulisha mpaka sasa. Wengine ni Lazarus Kambole na Gael Bigirimana
Bado nyota wawili wa kigeni wanasubiri utambulisho ambao ni mlinzi wa kushoto Mcongomani Joyice Lomalisa na kiungo mshambuliaji Stephane Aziz Ki