Leo majira ya saa tisa Alasiri mabingwa wa soka Tanzania Bara Yanga watashuka kunako uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha kuikabili Coastal Union katika mchezo wa fainali michuano ya kombe la Shirikisho la Azam (ASFC)
Yanga inawania rekodi ya aina yake ya kushinda mataji matatu msimu huu pasipo kupoteza mchezo katika mashindano yote
Hata hivyo hautakuwa mchezo mwepesi kwani wanakutana na Coastal Union ambayo inawania nafasi ya kushiriki michuano ya Kimataifa mara ya mwisho wakishiriki mwaka 1989 wakati kocha wao wa sasa Juma Mgunda akiwa ni mchezaji wa timu hiyo
Hii itakuwa mara ya tatu timu hizo kukutana msimu huu, Yanga ikishinda michezo yote miwili waliyokutana kwenye ligi
Lakini mara nyingi mchezo wa fainali unakuwa na sura tofauti, ni dakika 90 au 120 za kujitoa kwa kila timu
Wananchi wataingia katika mchezo huo wakiwa na kikosi chao kamili, Nabi aliwapa mapumziko baadhi ya wachezaji kwenye mchezo wa mwisho kwenye ligi dhidi ya Mtibwa Sugar
Ni mchezo mgumu lakini Yanga inapewa nafasi kubwa ya kuibuka na ushindi kutokana na ubora wa kikosi chao
Yanga imedhihirisha umwamba msimu huu kwa kutwaa ubingwa wa ligi kuu mapema lakini pia wakicheza msimu mzima pasipo kupoteza mchezo