Mwenyekiti wa Yanga Dk Mshindo Msolla amesema mafanikio waliyopata msimu huu yametokana na sapoti kubwa waliyopata kutoka kwa wadhamini hivyo Wananchi wana kila sababu ya kuwaunga mkono wadhamini wao
Dk Msolla amewataja wadhamini wakuu Sportpesa lakini pia kwa umuhimu wa kipekee akawataja GSM, Taifa Gas na Azam Media kuwa wamehusika kwenye mafanikio ambayo Yanga wanajivunia msimu huu
"Katika mafanikio haya hatuwezi kukosa kuwataja watu hawa watatu; Kwanza GSM, amefanya mambo makubwa kutokana na mapenzi yake kwa klabu hii. Pili ni Taifa Gas na tatu ni Mzee Bakhressa (Azam Media). Tunamshukuru Bakhressa kwa kuonyesha ni Mwanamichezo, tulisaini mkataba wa miaka 10 wenye thamani ya Tsh Bilioni 41"
"Nawaambia mashabiki na Wanachama wa Yanga, tuwaunge mkono sana hawa watu, shukrani pekee ambayo tunaweza kuwapa ni kununua bidhaa zao," alisema Dk Msolla
Dk Msolla pia ametoa ufafanuzi kuwa haikuwa lazima kwake kuonekana kila eneo katika shamrashamra za ubingwa jijini Dar es salaam kwa kuwa usimamizi wa matukio yote ulikuwa chini ya Sekretariati
Dk Msolla atamaliza muda wake Julai 10 utakapofanyika uchaguzi wa kuwapata viongozi wapya wa Yanga
Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano Yanga Injinia Hersi Said anatarajiwa kuwa Rais wa Yanga akiwa mgombea pekee katika kinyan'ganyiro hicho