Licha ya kutopata muda wa kutosha kufanya maandalizi, Kocha Mkuu wa Yanga Nasreddine Nabi amesema vijana wake wako tayari kuwakabili Mbeya City katika mchezo wa ligi kuu ambao utapigwa uwanja wa Sokoine
Mchezo huo ambao utapigwa kesho Jumamosi, unatarajiwa kuanza mapema majira ya saa tisa na nusu ili kupisha shamrashamra za ubingwa ambao Yanga watakabidhiwa
Yanga iliwasili mkoani Mbeya jana na leo kufanya mazoezi ya mwisho kwenye uwanja wa Sokoine
Wananchi wametoka kucheza na Polisi Tanzania juzi katika dimba la Benjamin Mkapa na kufanikiwa kuibuka na ushindi wa mabao 2-0
"Tumecheza mechi mfululizo na itakuwa hivyo mpaka mchezo wa fainali kombe la FA. Tunafanya mazoezi maalum ya 'recovery' kuwaweka sawa wachezaji tayari kwa mchezo"
"Wachezaji wanafahamu mahitaji ya timu, mashabiki wanapenda kuona timu yao inashinda katika siku hii maalum kwetu hivyo tutapambana kuhakikisha tunawapa furaha," alisema Nabi
Yanga itakabidhiwa taji la ligi kuu baada ya mchezo huo na kuanza shamrashamra za ubingwa mkoani Mbeya
Kikosi kitaondoka Mbeya mapema Jumapili kurejea jijini Dar es salaam kuhitimisha sherehe hizo za ubingwa