Kocha Mkuu wa Yanga Nasreddine Nabi amemkaribisha winga Saimon Msuva katika kikosi cha Yanga wakati huu akiendelea kutatua mgogoro wake dhidi ya klabu ya Wydad Athletic
Msuva yuko nchini kwa miezi kadhaa sasa akiwa na mgogoro na Wydad akifungua kesi katika Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi wa Michezo (CAS)
Nabi ameeleza kuvutiwa na uchezaji wa Msuva na kubainisha kuwa litakuwa jambo jema kama mchezaji huyo atajiunga na Yanga
"Natamani sana kufanya kazi na yule Msuva, ni mchezaji mwenye kipaji kikubwa. Napenda sana kasi yake, juhudi lakini kitu bora zaidi anaweza kufunga na kucheza nafasi nyingi"
"Sisi ni mabingwa sasa hapa Tanzania, kwasasa najua Msuva ana shida na klabu yake, najua yataisha ila wakati huu ni kitu kizuri angekuja hapa Yanga aweze kupambana kujiweka sawa, atalisaidia taifa lake na hata sisi tutapata kitu," Nabi amenukuliwa na gazeti la Mwanaspoti
Msuva aliitumikia Yanga kwa mafanikio akiwa sehemu ya kikosi kilichotwaa ubingwa kwa misimu mitatu mfululizo kutoka 2014 mpaka 2017 na baadae Yanga ikamuuza klabu ya Difaa EL Jadid ya Morocco
Msuva aliitumikia Wydad kwa msimu mmoja tu kabla ya kuingia kwenye mgogoro ambao umemuweka nje kwa takribani miezi sita sasa
Hata hivyo mwenyewe amesema mgogoro huo utamalizika karibuni na ataweka hadharani hatma yake ingawa kama ataamua kubaki nchini ni wazi klabu atakayojiunga nayo ni Yanga
Mwezi Januari mwaka huu Msuva alitembelea kambi ya Yanga, Avic Town na kupata nafasi ya kuzungumza na wachezaji na benchi la ufundi. Rais mtarajiwa wa Yanga Injinia Hersi Said amekuwa mstari wa mbele kuhakikisha anamrudisha Msuva Jangwani






