Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mohamed Mchengerwa amesema serikali inakusudia kutumia Sh bilioni 10, kukarabati viwanja saba vya michezo, ili kuiwezesha Tanzania kukidhi vigezo vya kuandaa mashindano ya kimataifa na kikanda ikiwemo michuano ya AFCON 2027.
Akiwasilisha hotuba ya bajeti kwa mwaka wa fedha 2022/23 bungeni jijini Dodoma, Mchengerwa ametaja viwanja hivyo kuwa ni pamoja na Jamhuri-Dodoma, Sheikh Amri Abeid - Arusha, Sokoine - Mbeya, CCM Kirumba; Mwanza, na Mkwakwani - Tanga.
"Ukarabati huo pia utavihusisha viwanja vya Uhuru na Benjamina Mkapa jijini Dar es Salaam. Hatua ya pili ni kukarabati viwanja vingine ikiwa ni pamoja na kuweka nyasi bandia na majukwaa katika mikoa ya Kigoma, Rukwa, Mtwara, Iringa, Tabora na Shinyanga baada ya kujadiliana na wamiliki wa viwanja hivyo"
"Mkakati huu utaiwezesha Tanzania kufanikisha maandalizi ya kuwa mwenyeji wa mashindano ya AFCON, ambayo tayari Tanzania imependekezwa kwa mwaka 2027 ambayo ni ndoto ya Rais, Samia Suluhu Hassan ya kuandaa mashindano makubwa ya michezo," alisema Waziri Mchengerwa