Kambi ya Yanga mkoani Shinyanga imekuwa na mafanikio makubwa timu ikipata utulivu waliouhitaji katika maandalizi yao ya mchezo wa nusu fainali kombe la Shirikisho la Azam (ASFC) dhidi ya Simba ambao utapigwa kesho Jumamosi May 28 katika uwanja wa CCM Kirumba
Msemaji wa Yanga Haji Manara amesema kambi hiyo imewapa morali ya kuelekea jijini Mwanza kifua mbele, wakiwa na matumaini ya kushinda mchezo huo unaotarajiwa kuwa na ushindani mkali
Manara amesema wanafahamu ugumu wa kucheza mechi ya nusu fainali dhidi ya wapinzani wao wakubwa lakini wamejipanga kutimiza malengo waliyojiwekea msimu huu
"Tunajua ugumu wa kucheza na wapinzani ambao pia ni watani zetu, lakini Sisi ni Yanga, tuna malengo mahsusi msimu huu na tunakaribia kuyatimiza"
"Tutacheza kwa nidhamu kubwa ya mchezo bila Kurudi nyuma, tutawaheshimu wachezaji wao bila kuwaogopa, tutacheza Kwa niaba ya Wananchi wa nchi hii wenye matumaini makubwa na timu yao"
"Mechi hii haina matokeo ya sare, Makocha na Wachezaji wetu wanalijua hilo. Tutakuwa zaidi ya Yanga muijuayo, kwa nini isiwe hivyo ilhali tumethibitisha hayo msimu mzima?"
"Washabiki wetu mje kusapoti mabingwa wa hili Taifa, mje mmevaa jezi zenu, Mliopo Majumbani mtuombee bila kuwanga, Mungu pekee ndio huombwa, " alisema Manara
Yanga inatarajiwa kuelekea jijini Mwanza mapema kesho tayari kwa mchezo huo ambao utapigwa kuanzia saa 9:30 Alasiri