Vinara wa ligi kuu ya NBC Yanga jioni ya leo wanashuka uwanja wa CCM Kirumba kuikabili Biashara United katika mchezo wa ligi raundi ya 26
Baada ya watani zao Simba kudondosha alama mbili katika uwanja huo hapa jana kwa kulazimishwa sare ya bao 1-1 dhidi ya Geita Gold, Yanga inahitaji alama nne kutoka mechi tano zilizobaki kutwaa ubingwa
Ni wazi Kocha Nasreddine Nabi angependa kuona vijana wake wanatwaa ubingwa mapema inavyowezekana ili kupunguza presha katika mechi za mwishoni
Leo Yanga itaingia uwanja wa CCM Kirumba ikiwa na dhamira moja tu, kushinda mchezo huo ili kufikisha alama 66 ambazo zinaweza pia kuwahakikishia ubingwa
Nabi anatarajiwa kuwarejesha kikosini baadhi ya wachezaji ambao aliwapa mapumziko katika mchezo uliopita dhidi ya Mbeya Kwanza
Djuma Shabani alikosa mchezo uliopita akitumikia adhabu ya kadi tatu za njano, anatarajiwa kurejea kikosini leo kama ilivyo kwa Feisal Salum 'Fei Toto' na nahodha Bakari Nondo Mwamnyeto waliopumzishwa mchezo uliopita
Chico Ushindi alitumika kwa takribani dakika 30 katika mchezo uliopita, leo anaweza kupewa muda mrefu zaidi
Yacouba Songne ameshiriki kikamilifu mazoezi ya mwisho ya Yanga kuelekea mchezo huo, pengine leo anaweza kupata dakika chache kumrejesha uwanjani baada ya kuwa nje kwa takribani miezi mitano
Jambo jema ni kuwa Yanga itaingia katika mchezo huo ikiwa na kikosi chake kamili, hakuna majeruhi na ushindi utawaweka katika wakati mzuri sana kuelekea mchezo wa nusu fainali kombe la FA dhidi ya Simba ambao utapigwa Jumamosi hapo CCM Kirumba