Alama sita zimesalia kwa Yanga kutwaa ubingwa wa ligi kuu msimu huu baada ya leo kuichapa Mbeya Kwanza mabao 4-0 katika mchezo uliopigwa uwanja wa Benjamin Mkapa
Yanga iliingia katika mchezo huo ikiwa na dhamira moja, kuzisaka alama tatu muhimu kuelekea ubingwa
Mbeya Kwanza waliingia katika mchezo huo kwa kujilinda zaidi lakini mbinu yao ilivurugwa na Yanga kwenye dakika ya 34, Fiston Mayele akifunga bao lake la 13 baada ya krosi murua kutoka kwa Salum Abubakar 'Sure Boy'
Kuingia kwa bao hilo kuliifanya Yanga iongezea mashambulizi langoni kwa Mbeya Kwanza na kufanikiwa kufunga mabao mengine mawili kabla ya mapumziko kupitia kwa Saido Ntibazonkiza na Dickson Ambundo
Yanga iliendelea kutawala mchezo katika kipindi cha pili ambapo kwenye dakika ya 60 kocha mkuu wa Yanga Nasreddine Nabi alifanya mabadiliko kwa kuwaingiza wachezaji wanne Chrispine Ngushi, Chico Ushindi, Heritier Makambo na Zawadi Mauya
Makambo akafunga bao lake la kwanza msimu huu kwenye dakika ya 72 akiunganisha pasi ya kichwa kutoka kwa Ushindi
Ulikuwa mchezo ambao Yanga ingeweza kufunga mabao mengi zaidi kama wangetumia vyema nafasi nyingi walizotengeneza
Yanga sasa imefikisha alama 63 ikiongoza ligi kwa tofauti ya alama 13 dhidi ya Simba inayoshika nafasi ya pili
Ushindi katika michezo miwili ijayo itatosha kuipa Yanga ubingwa
Aidha kama Simba itapoteza mchezo dhidi ya Geita Gold Jumapili, Yanga inaweza kutwaa ubingwa Jumatatu kama watapata ushindi dhidi ya Biashara United




