Kocha Mkuu wa Yanga Nasreddine Nabi amesema huu sio wakati wa kusherehekea ubingwa wa ligi kuu kwani bado hawajashinda
Akizungumza katika Mkutano na Wanahabari kuelekea mchezo dhidi ya Mbeya Kwanza ambao utapigwa Ijumaa katika uwanja wa Banjamin Mkapa, Nabi amesema bado wana kazi ya kufanya kuhakikisha wanapata matokeo mazuri katika michezo iliyobaki
"Bado ubingwa Yanga, bado.. Subiri kidogo sio wakati wa kusherehekea, pale wakati utakapofika tuwe na alama ambazo zinatuhakikishia kuwa bingwa basi tutasherehekea lakini kwa sasa bado," alisema Nabi
Akizungumzia maandalizi ya kikosi chake kuelekea mchezo huo wa Mbeya Kwanza, Nabi amesema wamejiandaa kuhakikisha wanapata ushindi
Hata hivyo Nabi amesema katika siku tisa wanakabiliwa na michezo mitatu hivyo watalazimika kufanya mabadiliko ya wachezaji kulingana na utayari wao
"Tuna mechi tatu katika siku tisa hivyo mashabiki wasishangae kama wataona kuna wachezaji wanaanza na wengine wanabaki nje, tunapaswa kutumia wachezaji wengi ili kuhakikisha hatuathiriwi na uchovu"
Baada ya mchezo dhidi ya Mbeya Kwanza, Yanga itasafiri mkoani Mwanza kuifuata Biashara United kwa ajili ya mchezo ambao utapigwa May 23
Kikosi kitaweka kambi jijini Mwanza kujiandaa na mchezo wa nusu fainali kombe la FA dhidi ya Simba ambao utapigwa May 28 katika uwanja huohuo wa CCM Kirumba