Kocha Mkuu wa Yanga Nasreddine Nabi amesema benchi la ufundi, wachezaji wanatambua umuhimu wa ushindi kwenye mchezo ligi kuu dhidi ya Dodoma Jiji ambao utapigwa uwanja wa Jamhuri mkoani Dodoma hapo kesho
Nabi amesema wanajua timu inapita katika wakati mgumu baada ya kukosa ushindi katika michezo mitatu iliyopita, ni muhimu sana kwao kupata matokeo mazuri katika mchezo huo
"Tumekuwa na msimu mzuri licha ya kuwa katika michezo mitatu iliyopita hatukupata ushindi. Ni muhimu sana kwetu kuhakikisha tunapata matokeo mazuri. Hatuna wasiwasi, tunaamini uwezo wa wachezaji wetu"
"Tunawaomba mashabiki wetu waje kwa wingi kutuunga mkono kama walivyofanya tangu mwanzo wa msimu. Hiki ni kipindi ambacho wanahitaji kuwapa moyo wachezaji naamini tutaweza kufanikiwa malengo yetu ya kutwaa ubingwa msimu huu," alisema Nabi ambaye katika Mkutano na Wanahabari aliongozana na kocha Msaidizi, Cedric Kaze
Akizungumzia hali ya kikosi chake kuelekea mchezo huo, Nabi amesema wachezaji wawili tu ndio hawako katika mpango wa mchezo
"Yacouba Songne tutaendelea kumkosa, anaendelea kuimarika baada ya kupata majeraha yaliyomuweka nje kwa muda mrefu. Pia tutamkosa Chico Ushindi ambaye licha ya kuwa amepona, hatudhani kama yuko tayari kwa mchezo huo"
"Yannick Bangala yeye amepata msiba(kafiwa na kaka yake), tutazungumza nae kuona kama ataweza kushiriki mchezo huo, hili litategemea na saikolojia yake"
Nabi amesema wanafahamu Dodoma Jiji ni moja ya timu imara kwenye ligi kuu msimu huu licha ya kuwa hawajawa na mwendelezo mzuri wa matokeo
Amesema vijana wake watapigana vita mbili hapo kesho, kusaka ushindi dhidi ya Dodoma Jiji katika uwanja ambao sio bora