Kocha Mkuu wa Yanga Nasreddine Nabi amewataka mashabiki wa timu hiyo kuwapa moyo wachezaji kuhakikisha wanapambana kupata matokeo katika michezo saba iliyobaki
Nabi amesema kilichowakosesha ushindi katika mchezo dhidi ya Prisons ni bahati tu kwani walitengeneza nafasi nyingi ambazo zingeweza kuwapa ushindi mnono
Nabi amesema ana imani kubwa na wachezaji wake, ushirikiano na mshikamano wa viongozi, benchi la ufundi, wachezaji na mashabiki utawahakikishia kuwa mabingwa msimu huu
"Tunawaomba radhi mashabiki wetu kwani tumekosa ushindi katika michezo mitatu iliyopita. Tulikuwa na nafasi nzuri ya kupata ushindi mchezo dhidi ya Prisons lakini haikuwa bahati, ni matokeo ya mpira wa miguu"
"Hatupaswi kuwaongezea presha wachezaji, tumekosa matokeo kama timu na tunapaswa kuangalia wapi tulikosea na kusonga mbele. Tunapaswa kuhakikisha tunafanya vizuri katika michezo saba iliyobaki bila ya kuangalia matokeo ya mpinzani wetu. Kama tutaanza kufarakana wenyewe tutawapa nafasi wapinzani," alisema Nabi
Aidha Nabi amemtetea mshambuliaji Fiston Mayele aliyekosa mkwaju wa penati akisema hilo ni jambo la kawaida kwani hakuna mchezaji ambaye hajawahi kukosa penati
"Mayele alichukua mpira kwa sababu alikuwa akijiamini anaweza kufunga, wenzake walimuachia kwa sababu walimuamini pia, hivyo ni bahati mbaya kwake kukosa. Lakini pia tulikosa nafasi nyingine za wazi kupitia kwa Feisal, Moloko na Makambo"
"Itoshe kusema wachezaji walipambana na kutengeneza nafasi nyingi hatukuweza kufunga, tutaanzia hapo kujisahihisha ili tufanye vizuri katika michezo iliyobaki"