Waswahili wanasema punda afe lakini mzigo lazima ufike, ndivyo ambavyo Yanga inapaswa kuikabili michezo saba iliyobaki kuhitimisha msimu huu
Matokeo ya suluhu ya bila kufungana dhidi ya Tanzania Prisons leo ni wazi yameongeza presha, lakini wachezaji hawapaswi kushusha morali yao kwani bado wana kazi ya kufanya
Yanga imekosa ushindi leo, mkakati uwe kushinda mchezo unaofuata, haya matokeo ya leo yamepita
Ilitarajiwa michezo ya mwishoni itakuwa migumu sana kwa sababu kila timu itaingia katika mchezo huo ikiwa na malengo
Timu 14 ziko katika hatari ya kuteremka daraja hivyo kila mchezo uliobaki una hadhi ya fainali
Kocha Nasreddine Nabi atakuwa na kazi ya kufanya kwenye viwanja vya mazoezi kuhakikisha vijana wake wanaongeza umakini katika michezo ijayo
Mchezo wa leo Yanga ingeweza kuondoka na ushindi mnono kama wachezaji wangeongeza umakini kidogo tu katika kipindi cha kwanza
Hesabu bado ziko salama kwa Yanga, wako kileleni mwa msimamo wa ligi kwa tofauti ya alama 11, hata ikitokea Simba ameshinda kiporo chake, zitabaki alama nane