Ili kuhakikisha wanafikia malengo, Kocha Mkuu wa Yanga, Nesreddine Nabi amewataka wachezaji wa timu hiyo kupambana na kufikiria kama wanaanza msimu ili kupata matokeo mazuri katika michezo yao nane iliyobakia ya Ligi Kuu ya NBC
Katika mechi hizo nane zilizobakia, Yanga ambao ndio vinara inahitaji kushinda michezo mitano ili kutangazwa mabingwa wapya wa msimu huu bila ya kuangalia matokeo ya timu nyingine yoyote.
Michezo iliyobaki ni dhidi ya Tanzania Prisons, Dodoma Jiji, Mbeya Kwanza, Biashara United, Coastal Union, Polisi Tanzania, Mbeya City na Mtibwa Sugar.
Nabi amesema wachezaji wanahitaji kubadili fikra zao wakiamini wameshamaliza kazi kutokana na namna walivyocheza katika michezo miwili iliyopita dhidi ya Simba na Ruvu Shooting.
Nabi alisema bado hawajafikia malengo ya kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara na baada ya kutoka suluhu na Simba wachezaji wakawa wameridhika jambo ambalo halijamfurahisha.
"Wachezaji wanatakiwa kujitoa na kupambana zaidi ya hapo, lengo ni kutwaa ubingwa wa ligi, sitaki kuona mchezaji yoyote anacheza kwa kuridhika na kuondoa ule ubora wake aliokuwa nao kabla ya mchezo dhidi ya Simba,” alisema Nabi
Alisema anahitaji wachezaji kujitoa zaidi katika michezo iliyobaki ili kuzipata pointi hizo wanazozihitaji ambazo hazitafikiwa na timu yoyote katika mbio hizo za kuwavua ubingwa
Kocha huyo alisema wanahitaji kuweka rekodi nyingine ikiwamo kuchukua ubingwa kwa idadi kubwa ya pointi na mabao mengi ya kufunga pia ikiwezekana wamalize msimu bila ya kupoteza mechi hata moja.
"Baada ya kurejea jijini, tutarudi uwanjani kwa ajili ya kufanyia kazi mapungufu yaliyojitokeza katika michezo miwili iliyopita na kujiweka sawa na mechi iliyopo mbele yetu dhidi ya Tanzania Prisons," alisema kocha huyo.
Yanga itashuka tena dimbani keshokutwa kuwakaribisha Tanzania Prisons kuanzia saa 1:00 usiku kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam.