Baada ya kurejea kutoka mkoani Kigoma hapo jana, kikosi cha Yanga leo kinatarajiwa kuanza maandalizi ya mchezo unaofuata dhidi ya Tanzania Prisons
Jumatatu, May 09 vinara hao wa ligi kuu watashuka uwanja wa Benjamin Mkapa kuikabili Tanzania Prisons katika mchezo ambao alama tatu kwa Yanga zitakuwa na maana kubwa katika mkakati wao wa kutwaa ubingwa msimu huu
Kimahesabu, Yanga inahitaji alama 15 tu kutoka michezo nane iliyobaki ili kujihakikishia kutwaa ubingwa
Alama 15 zitaifanya Yanga ifikishe alama 71, alama ambazo hazitaweza kufikiwa na timu nyingine yoyote
Simba inayoshika nafasi ya pili, kama itashinda michezo yote tisa iliyobaki, itafikisha alama 70
Wananchi wanaweza kukamilisha jambo lao mwezi huu kama watashinda mechi nne zilizobaki kwa mwezi May
Baada ya mchezo dhidi ya Tanzania Prisons, Yanga itaelekea mkoani Dodoma kuikabili Dodoma Jiji May 15 kisha kurudi Dar kuikabili Mbeya Kwanza May 21
May 24 Wananchi watasafiri mkoani Mwanza kuifuata Biashara United kwa ajili ya mchezo ambao utapigwa uwanja wa CCM Kirumba