Baada ya mchezo dhidi ya Simba uliopigwa uwanja wa Benjamin Mkapa jana na kumalizika kwa suluhu ya bila kufungana, Yanga inahitaji takribani pointi 18 kutoka michezo tisa iliyobaki kutwaa ubingwa
Baada ya mchezo dhidi ya Simba, Yanga imefikisha alama 55 baada ya kushuka dimbani mara 21 huku Simba ikibaki na alama 42 baada ya kushuka dimbani mara 20
Yawezekana kabisa Yanga inaweza kutangaza ubingwa katika michezo mitano inayofuata kama itaweza kushinda na kama wapinzani wao watakosa ushindi angalau mchezo mmoja katika michezo mitano inayofuata
Jumatano May 04 Yanga watakuwa mkoani Kigoma kuikabili Ruvu Shooting kisha watarejea jijini Dar es salaam kuikabili Tanzania Prisons katika mchezo utakaopigwa uwanja wa Benjamin Mkapa May 09
Baada ya mchezo huo, Wananchi wataelekea mkoani Dodoma kuifuata Dodoma Jiji katika mchezo ambao utapigwa May 15 katika uwanja wa Jamhuri
May 21 Wananchi watakuwa Dar kuikaribisha Mbeya Kwanza na baadae kusafiri mkoani Mwanza kuifuata Biashara United katika mchezo ambao utapigwa May 24 kunako dimba la CCM Kirumba
Watani zao Simba michezo yao mitano inayofuata kwenye ligi ni dhidi ya Namungo Fc (ugenini), Ruvu Shooting (nyumbani), Kagera Sugar (nyumbani), Azam Fc (ugenini) na Geita Gold (ugenini)
Namungo Fc, Azam Fc na Geita Gold zote zinawania kumaliza nafasi ya tatu kwenye msimamo wa ligi ili kujipatia mamilioni ya Azam TV na zaidi kushiriki michuano ya CAF msimu ujao
Hivyo ni wazi kwa Simba michezo hiyo haitakuwa rahisi kwao. Yanga ilifanikiwa kushinda michezo yote mitatu dhidi ya timu hizo