Kocha Mkuu wa Yanga Nasreddine Nabi hana kazi kubwa katika uchaguzi wa kikosi chake kitakachoikabili Simba katika mchezo wa ligi kuu ya NBC leo
Karibu wachezaji wote wako tayari kwa mchezo huo, ni jukumu la Nabi na benchi lake la ufundi kuamua
Hakuna shaka Fiston Mayele leo ataongoza safu ya ushambuliaji huku akisaidiana na Feisal Salum au Stephane Aziz Ki
Mayele yuko kwenye kiwango bora sana akifunga mabao 12 katika mechi 10 zilizopita kwenye mashindano yote
Bernard Morrison anakosekana leo hivyo ni wazi katika nafasi yake Farid Mussa au Tuisila Kisinda mmoja anaweza kuingia
Jesus Moloko anatarajiwa kuendeleza kasi yake upande wa winga wa kulia wakati Khalid Aucho na Yannick Bangala huenda wakasimama eneo la kiungo
Katika mchezo uliopita dhidi ya Al Hilal Bangala alirudishwa kwenye safu ya kiungo baada ya kutumika eneo la ulinzi katika mechi zote zilizopita msimu huu
Djuma Shabani yuko fiti na leo ataendeleza kutengeneza mabao upande wa kulia wakati Kibwana Shomari atakuwa na kazi maalum kwenye safu ya ulinzi upande wa kushoto
Nahodha Bakari Mwamnyeto na Dickson Job wanaweza kuendelea kuilinda ngome wakiwa walinzi wa kati
Djigui Diarra amekuwa kiongozi katika safu ya ulinzi, hakuna shaka leo atakuwa na kazi ya kuhakikisha lango la Yanga linabaki salama kwa dakika zote 90
Huu ni mchezo muhimu kwa Yanga kupata ushindi ili kurudi kileleni katika msimamo wa ligi