Jana baada ya mchezo dhidi ya Namungo Fc uliomalizika kwa Yanga kuibuka na ushindi wa mabao 2-1, kocha msaidizi wa Yanga Cedric Kaze alifichua kuwa walitumia maneno ya kocha msaidizi wa Namungo Fc Jamhuri Kiwhelo 'Julio' aliyoyatoa siku moja kabla ya mchezo kuwaongezea morali wachezaji
Kaze ambaye alikiri kuwa hakuwa akifahamu kama Julio ni kocha kabla ya kumuona katika benchi la ufundi la Namungo Fc, alisema kauli za Julio ziliwaongezea wachezaji wake ari ya kushinda mchezo huo
"Tulimsikia mshabiki wa ile timu nyingine akisema wanataka kutufunga ili wapunguze tofauti ya pointi kati yetu na Simba halafu akiamini tunaweza kufungwa na Simba na tofauti ya pointi kuwa nne"
"Tuliwaonyesha video wachezaji wetu kabla ya mchezo na wao kuona wanahitaji kushinda mchezo huu. Nimeshangaa kumuona kwenye benchi la ufundi (Julio), sikufahamu kama ni kocha kwani siamini kama kocha wa mpira unaweza kutoa kauli za aina ile," alisema Kaze
Aidha Kaze alipongeza kiwango bora kilichoonyeshwa na wachezaji akiutaja mchezo huo kama mechi bora walizocheza msimu huu
"Nawapongeza wachezaji kwa mchezo mzuri, tulikuwa na kiwango bora sana. Hii ni aina ya michezo ambayo tungeweza kufunga mabao matano, sita na hata saba kama tungekuwa makaini zaidi. Tulipaswa kumaliza mchezo huu tangu kipindi cha kwanza lakini muhimu zaidi tumeweza kupata alama tatu"
"Sasa tunakwenda kwenye mchezo unaofuata dhidi ya Simba tukiwa na dhamira ya kushinda ili tufute matumaini ya wapinzani wetu katika mbio za kuwania ubingwa"