Yanga inaendelea kutamba kileleni mwa msimamo wa ligi kuu ya NBC wakiwa na alama zao 51 baada ya michezo 19
Ni alama 10 zaidi ya timu inayofuata katika nafasi ya pili, Simba yenye alama 41 pia wakiwa wameshuka dimbani mara 19
Kwa mashabiki wa Yanga, kiu ya kutwaa ubingwa wa ligi kuu ni kubwa hasa baada ya kuukosa kwa misimu minne mfululizo
Kuna kila dalili Wananchi wanaweza kuurejesha ubingwa huo Jangwani kwa mara ya 28 msimu huu, pengine jambo hilo linaweza kutimia mapema
Michezo mitano inayofuata katika ratiba, inaweza kutosha kuwapa Yanga ubingwa kama watazichanga karata zao vyema huku wakiomba watani zao Simba waache alama katika baadhi ya mechi zao
Habari njema ni kuwa michezo yote mitano inayofuata itapigwa uwanja wa Benjamin Mkapa kama hakutakuwa na mabadiliko kwenye mchezo dhidi ya Ruvu Shooting
April 30 wananchi watashuka uwanja wa Benjamin Mkapa kuikabili Simba katika mchezo ambao matokeo ya ushindi yatawafanya waongeze tofauti ya pointi kuwa 13
Baada ya mchezo huo, Yanga itarudi uwanja wa Benjamin Mkapa May 04 kuikabili Ruvu Shooting, Ruvu watakuwa wenyeji wa mchezo huo (mpaka sasa ratiba inaonyesha utapigwa uwanja wa Mkapa)
Michezo itakayofuata ni dhidi ya Namungo Fc, Tanzania Prisons na Mbeya Kwanza yote Yanga akiwa mwenyeji hivyo itapigwa kwa Mkapa
Ratiba ya watani zao Simba inaonyesha baada ya mchezo dhidi ya Yanga, May 03 watasafiri mkoani Lindi kuifuata Namungo Fc kisha kurejea jijini Dar es salaam kuzikabili Ruvu Shooting na Kagera Sugar
Kisha watasafiri mkoani Mwanza kuifuata Geita Gold na baadae kurudi Dar kuzikabili KMC na Azam Fc