Kiungo wa Yanga, Salum Abubabakar 'Sure Boy' ameeleza furaha yake kucheza tena kwenye uwanja aliouzoea wa Azam Complex, Chamazi akiwa na timu yake mpya, huku akipata ushindi wa mabao 2-1
Sure Boy amesema kwake ilikuwa ni mechi yenye hisia, kwani alikuwa akicheza dhidi ya timu iliyomlea, na timu yake mpya, pia kwenye uwanja ambao ameuzoea sana
"Tumepata pointi tatu, mechi ilikuwa ngumu, timu zote tulicheza vizuri, pale kati tulikuwa na kazi kwa sababu wote tulikuwa tunafahamiana, mimi nimecheza kwenye timu ya Azam na wachezaji waliokuwa wanacheza nafasi ya kiungo, kwa hiyo kila mmoja alikuwa anaonyesha nini anacho mguuni"
"Si kweli kama tulikuwa tumekamiana sana kama baadhi ya watu wanavyosema. Wao wameuzoea uwanja na mimi pia nimeuzoea pia na tumezoeana hata mazoezi tulikuwa tunacheza wote, kwa hiyo ilikuwa ni kazi kubwa pale katikati, naamini tulicheza vizuri wote, mimi nilitaka kuonyesha vitu na wao hawakuniacha, ila hatukukamiana," alisema.
Sure Boy amekuwa na kiwango kizuri tangu alipojiunga na Yanga katika dirisha dogo la usajili mwezi Januari mwaka huu (2022) akitokea klabu ya Azam Fc ambayo aliitumikia kwa miaka 14